Mwigizaji wa Tanzania Wema Sepetu anajuta baada ya kuandaa sherehe ya siku yake ya kuzaliwa na mambo kwenda kinyume na matarajio yake kwenye hafla hiyo.
Kidosho huyo kipenzi cha Tanzania alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kutoa taarifa ambapo alisema madhumuni ya kuandaa sherehe yalikuwa kufurahia na awapendao lakini haikuwa alivyotarajia.
“Kwa kifupi shughuli yangu iliharibika sana. Lengo langu halikutimia. Nimejitahidi kufanya kitu kizuri ambacho kingenifurahisha sana siku ya kuzaliwa kwangu ila haijakuwa. Ninajiskia vibaya sana.” ndiyo baadhi ya maneno aliyochapisha Wema.
Wema aliapa kutoandaa tena sherehe ya siku ya kuzaliwa akisema hii ya mwisho ilikuwa mbaya sana. Alisisitiza kwamba aliumia moyo.
Lalama za Wema zinaaminika kuchochewa na hatua ya mamake mzazi ya kuonyesha kutoridhika kwake hadharani na uhusiano wa kimapenzi kati ya Wema na mwanamuziki Whozu.
Wakati wa kutoa hotuba, mamake Wema ambaye alikuwa amejawa hamaki alimzomea mwanawe akisema kwamba watoto wanapoingia kwenye mahusiano wanastahili kuheshimu wazazi.
Inaonekana kwamba Wema hajawahi kumtambulisha Whozu kwa mamake rasmi ndiposa akalalamika hivyo. Mzazi huyo alisema kwamba alistahili kufahamishwa wakati uhusiano huo wa kimapenzi ulianza.
Inadaiwa kwamba Whozu anaishi nyumbani kwa Wema na ndicho kitu ambacho kinamkera sana mamake Wema.
Lakini baada ya kumtupia maneno makali, mamake Wema alimhakikishia kwamba anampenda na atazidi kumpenda.