Waziri wa zamani Oloo Aringo ameaga dunia

Tom Mathinji
1 Min Read
Aliyekuwa mbunge wa Alego Usonga Oloo Aringo ameaga dunia.

Waziri wa zamani Peter Oloo Aringo ameaga dunia.

Aringo ambaye pia alikuwa mbunge wa Alego Usonga alifariki Novemba 1, 2024 akipokea matibabu katika hospitali moja Jijini Nairobi.

Habari kuhusu kifo cha Aringo, zilitolewa na naibu mkuu wa utumishi wa umma Eliud Owalo, kupitia mtandao wa X.

“Ni kwa huzuni na mshangao mkubwa nimefahamu kufariki kwa aliyekuwa waziri Peter “Castro” Oloo Aringo,” alisema Owalo.

“Mapema mwaka huu, mnamo Januari 14, nilimtembelea Oloo Aringo nyumbani kwake Jijini Nairobi ambapo tulijadili maswala mbali mbali,” aliongeza Owalo.

Owalo alimtaja Aringo kuwa waziri aliyekuwa na hekima ya kupigiwa mfano, na aliyechangia kubuniwa kwa tume ya wafanyakazi wa bunge PSC.

Aringo alihudumu bungeni kati ya mwaka 1974 na 1988, na kutoka mwaka 1997 hadi mwaka 2002.

Alikuwa waziri wa elimu wakati wa utawala wa serikali ya Rais Daniel Arap Moi, ambapo anasifiwa kwa kufanyia marekebisho mfumo wa elimu wa 8-4-4.

“Naungana na familia, marafiki na watu wa  Alego kumuomboleza Aringo,” alisema Owalo.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article