Waziri wa Elimu katika kaunti ya Machakos Philip Mutua Kilonzo amefutwa kazi.
Gavana Wavinya Ndeti anasema alichukua hatua ya kumpiga Kilonzo kalamu baada ya kubaini kuwa hana makali yanayotakikana ya kutekeleza majukumu yake katika wadhifa huo.
“Nimepitia upya utendakazi wake na kufikia hitimisho kuwa haiwezekani kwa yeye kuendelea kuhudumu kama waziri. Uamuzi huu umetokana na haja ya kudumisha viwango vya juu vya utoaji huduma kwa watu wa Machakos,” alisema Ndeti katika taarifa leo Jumatatu mchana.
Dkt. Consolata Mutisya sasa ndiye Waziri mpya wa Elimu wa kaunti hiyo.
Kabla ya kuhamishiwa Wizara hiyo, Dkt. Mutisya alihudumu kama Waziri wa Barabara, Uchukuzi na Ujenzi wa kaunti hiyo. Haijabainika ni lini wadhifa huo utajazwa.
Kilonzo alipigwa kalamu mwezi mmoja baada ya Gavana Ndeti kulifanyia mabadiliko Baraza lake la Mawaziri.
Katika mabadiliko hayo, Kilonzo alihamishiwa Wizara ya Elimu kutoka ile ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Miji na Nishati.
Kilonzo ni Waziri wa pili kuligura Baraza la Mawaziri la Gavana Ndeti baada ya aliyekuwa Waziri wa Michezo na Jinsia Onesmus Muasya kujiuzulu kwa sababu za kibinafasi.