Rais wa Costa Rica Laura Fernandez amemwachisha kazi Waziri wa Mambo ya Nje Manuel Tovar kwa kuhudhuria kikao cha usalama kilichoongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump bila idhini yake, hali iliyomzuia kuhudhuria.
Fernandez alisema kuwa ni yeye aliyepaswa kuhudhuria mkutano huo wa kukabiliana na walanguzi wa mihadarati na uhalifu wa kupangwa wala siyo Waziri wake.
Kulingana na taarifa hiyo, Waziri Tovar alikiuka itifaki kwani hakupaswa kuhudhuria mkutano huo bila kumjuza Rais.
Marais kadhaa wa mrengo wa kulia kutoka Amerika Kusini walihudhuria mkutano huo uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la 81 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA jijini New York.
Mataifa wanachama 15 yalisaini maafikiano ya kuzuia mali, kuwanyima viza na kuwahukumu watu 24 wanaoongoza na kuunga mkono makundi ya uhalifu.
Costa Rica, ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii Amerika Kusini, inakabiliwa na visa vingi vya ulanguzi wa mihadarati.
Waziri Tovar alimshukuru Rais Fernandez kwa kumjumuisha katika Baraza la Mawaziri huku akikwepa kuzungumzia kutimuliwa kwake.