Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya leo aliongoza shughuli ya upanzi wa miche katika eneo la Dongo Kundu kaunti ya Kwale.
Shughuli hiyo iliyopelekea miche elfu 60 ya mikoko kupandwa ilihusisha kundi la maafisa wa vikosi vya ulinzi vya Kenya, KDF kutoka kambi ya Mariakani wakiongozwa na kamanda brigedia Douglas Mokwena na wafanyakazi wa wizara wasio wanajeshi.
Zoezi hilo ni la kuchangia mpango wa serikali ya taifa wa kuhakikisha upanzi wa miche bilioni 15 kufikia mwaka 2032 na linachangia pia mpango wa kimazingira wa KDF.
Wakazi wa eneo hilo pia walihusika wakiongozwa na mbunge wa Kinango Gonzi Rai, makundi ya usalama ya kaunti ya Kwale yakiongozwa na naibu kamishna Lucy Ndemo na washirika kama huduma ya misitu, benki ya ABSA na wakfu wa Greens of Africa.
Waziri alisema mikoko inatekeleza jukumu muhimu katika mfumo ikolojia kwa kutoa eneo zuri la samaki kuzaliana. Hata hivyo aina hiyo ya miti iko katika hatari hasa kutokana na kuvunwa kupita kiasi na binadamu.
Hatua hiyo alisema inachangia kuharibiwa kwa misitu, huku akiitaka jamii ijiepushe na hulka ya kukata miti kuchoma makaa au kutumia vinginevyo kwani wanahujumu juhudi za kutunza mazingira.
Aliwasihi wakazi hao kuhakikisha kwamba miche iliyopandwa inakua kwa kuitunza huku akijitolea kuunga mkono juhudi zao za kupanda na kutunza miti.
Waziri Tuya aliwataka wadau wengine pia kusaidia jamii hiyo kwa kuinunulia miche watakayopanda.
Upanzi huo wa miche elfu 60, pia ni kwa heshima ya jeshi la wanamaji la Kenya linaloadhimisha miaka 60 tangu kubuniwa. Sherehe kuu itaandaliwa kesho Disemba 14, 2024.