Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Dkt. Margaret Ndung’u anasema Wizara yake ina mipango ya kubuni sera ya data na ile ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) kwa lengo la kuongoza nchi hii kuhusu namna ya kushughulikia mienendo inayoibuka ya teknolojia.
Sera hizo zinakuja wakati wizara tayari inaendeleza mkakati wa AI kwa lengo la kutoa mwongozo kwa teknolojia zinazoibuka kama vile teknolojia ya AI kwa kusudi la kutumia uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
“Katika dunia ya dijitali ya leo, dhana ya kukutanishwa kwa teknolojia, kujumuishwa kwa teknolojia mbalimbali kuwa mfumo mmoja, kumebadilisha namna tunavyoishi, kufanya kazi na kutangamana,” alisema Waziri Ndung’u alipoongoza hafla ya mahafali ya Chuo Kikuu cha Multimedia, MMU leo Ijumaa.
“Kukutanishwa huku kumekuwa nguvu inayosababisha uvumbuzi unaobadilisha utendakazi wa viwanda na kutoa changamoto kwa uendeshaji wa kawaida wa biashara.”
Waziri Ndung’u aliwakumbusha mahafali umuhimu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) katika kukuza maendeleo akisema ICT kwa sasa inaendesha karibu kila sekta zote za uchumi wa nchi ikiwa ni pamoja na afya, kilimo na biashara za mtandaoni na maongozi.
Alitoa mfano wa mfumo wa e-Citizen ambao umetumiwa kuhakikisha huduma za serikali zaidi ya 19,000 zinapatikana kwa njia ya mtandao na hivyo kurahisisha namna serikali inavyowahudumia raia.
“Maendeleo haya yanachochewa na upanuzi wa kimkakati wa miundombinu ya kidijitali ya Kenya, ikiwa ni pamoja na ajenda ya serikali ya uwekaji wa vituo vya kidijitali kote nchini, vinavyonuia kuhakikisha hata maeneo ya vijijini kabisa mwa nchi yetu yanapata huduma za Intaneti,” aliongeza Waziri huyo.
Dkt. Ndung’u alitoa wito kwa mahafali wa MMU kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ICT kupitia utafiti wao aliyosema utahakikisha suluhisho za kiteknolojia zinazopatikana zinasalia kuwa muhimu, jumuishi na zinazoweza kukidhi mahitaji yanayobadilika ya jamii.
Hii ilikuwa hafla ya 11 ya mahafali ya Chuo Kikuu cha MMU tangu kuasisiwa kwake na wanafunzi 1,600 walihitimu katika kozi mbalimbali wakati wa hafla hiyo.