Waziri wa Michezo Ababu Namwamba amesema mipango ipo ya kukamilisha ujenzi wa uwanja wa michezo wa Kamariny.
Akizungumza alipozuru uwanja huo ulioko Iten, kaunti ya Elgeyo Marakwet, waziri huyo alidokeza kuwa mwonekano na muundo wa uwanja huo utabadilishwa.
Aliandamana Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen na Gavana wa jimbo hilo Wisley Rotich.
Waziri Namwamba alitangaza ukarabati wa uwanja wa Iten ili kuinua hadhi yake hadi kiwango cha kuwa eneo la wanamichezo kuendelea kukuza talanta zao.
Hilo alisema linaambatana na mpango wa serikali wa #TalantaHela ambao lengo lake kuu ni kutambua na kukuza talanta na hatimaye kuzigeuza kuwa vitega uchumi.
Alitambua kaunti ya Elgeyo Marakwet kuwa nyumbani kwa wanamichezo wengi ambao wanafaa kupata mazingira bora ili kukuza na kuimarisha talanta zao.