Waziri Nakhumicha alaani kushambuliwa kwa wahudumu wa afya

Martin Mwanje
1 Min Read

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ameshutumu visa vya kushambuliwa kwa wahudumu wa afya nchini, akionya kuwa wanaotekeleza visa kama hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Onyo lake linawadia siku chache baada ya kusambaa kwa video mitandaoni iliyoonyesha mhudumu mmoja wa afya katika hospitali ndogo ya Port Victoria, kaunti ya Busia kuonekana akishambuliwa na raia.

“Visa vya dhuluma dhidi ya wahudumu wa afya si tu kwamba vinapaswa kulaaniwa bali pia havikubaliki. Wahudumu wa afya wanastahili kuheshimiwa kwani wao ndio uti wa mgongo wa mfumo wa afya,” amesema Waziri.

Nakhumicha alimsifia mhudumu wa afya aliyeshambuliwa wakati wa kisa hicho kwa kusalia mtulivu.

“Nampongeza mhudumu wa afya aliyehusika kwa kuonyesha kiwango cha juu cha utulivu na utaalam wakati wa tukio hilo. Hatuwezi tukaacha kusisitiza umuhimu wa kudumisha adabu wakati wa kutangamana na wahudumu wa afya.”

Vyama vya wahudumu wa afya nchini katika taarifa pia vimelaani kushambuliwa kwa wahudumu wa afya katika hospitali ya Port Victoria vikisema visa kama hivyo ni hatari kwa utendakazi wa wahudumu wa afya.

Aidha vimelalamikia kukithiri kwa visa vya kushambuliwa kwa wahudumu wa afya nchini na kutoa wito wa hatua madhubuti kuchukuliwa kuwalinda wahudumu wa afya.

 

 

Share This Article