Waziri wa Afya Susan Nakhumicha jana Jumatano usiku alifanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya kitaifa ya rufaa ya Kenyatta, KNH ili kutathmini utendakazi wake.
Wakati wa ziara hiyo iliyodumu saa moja na nusu, Nakhumicha alitembelea wodi za watoto na kina mama kujifungulia watoto.
“Ningependa kuupongeza usimamizi na wafanyakazi wa KNH kwa kudumisha utaratibu mwafaka na usafi wa hali ya juu hospitalini hapa,” alisema Waziri aliyewasifia wahudumu afya kwa kazi maridhawa wanayofanya akitoa mfano wa muuguzi Isaac Isamek.
“Wagonjwa niliokutana nao katika wodi za watoto na kina mama kujifungulia watoto waliridhishwa na huduma wanazopokea na waliisifia KNH.”
Hata hivyo, wauguzi waliokuwa zamuni walilalamikia idadi ndogo ya wahudumu wa afya wanaowahudumia wagonjwa wengi na uhaba wa vifaa tiba, lalama ambazo Waziri Nakhumicha aliahidi kuangazia.
Hospitali ya kitaifa ya rufaa ya Kenyatta, KNH ni hospitali kubwa Afrika Mashariki na Kati na hutoa huduma maalum wanaozhitaji wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali za bara hilo.