Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua amesema Kenya imejiandaa vilivyo kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tabia Nchi wa Afrika.
Mkutano huo wa siku mbili utaanza Septemba 4 na utaandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC jijini Nairobi.
Hii leo, Dkt. Mutua alikuwa katika hekaheka za kukutana na timu ya itifaki itakayokuwa mstari wa mbele kuwakaribisha wajumbe watakaoshiriki mkutano huo.
“Hii leo mchana, nilifanya mkutano na timu ya itifaki ya Wizara katika kujitayarisha kwa Mkutano wa Tabia Nchi ujao uliopangwa kufanyika kati ya Septemba 4 na 6, 2023 jijini Nairobi,” alisema Dkt. Mutua baada ya mkutano huo.
“Nina furaha kutangaza kuwa Kenya iko tayari kuwakaribisha wajumbe wote katika majadiliano haya muhimu ya mabadiliko ya tabia nchi.”
Serikali tayari imetangaza kuwa maafisa wa usalama wapatao 4,000 watapelekwa kudumisha usalama wakati wa mkutano huo.
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo amesema serikali pia imeandaa mpango madhubuti wa kuitikia hali za dharura zisizotazamiwa haraka iwezekanavyo.
Viongozi wa nchi mbalimbali ni miongoni mwa watu mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo.