Waziri Mutua asema mipango inaendelea ya kubinafsisha hoteli za serikali

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa utalii na wanyamapori Alfred Mutua amesema kwamba mipango inaendelea ya kubinafsisha hoteli ya Mombasa Beach ambayo iko chini ya hoteli zinazomilikiwa na serikali za Kenya Safari lodges.

Akizungumza katika hafla ya kila mwaka ya kutoa tuzo katika shuke ya Sheikh Zayed, waziri alisema kwamba anapanga kutekeleza mikakati mbali mbali ya kuimarisha utalii hasa katika eneo la pwani.

Kulingana naye kuanzishwa kwa vituo vya Halal vya kuvutia watalii kutaongeza idadi ya watalii kutoka nchi zilizo na waisilamu wengi na hivyo kuongeza mapato ya kigeni.

Mutua katika hotuba yake alihimiza serikali za kaunti kuhusika katika ubinafsishaji wa hoteli za serikali akisisitiza umuhimu wa uwazi katika mchakato mzima.

Alisema hata ingawa kuna upinzani kama vile hatua ya serikali ya kaunti ya Kakamega kutokubaliana na ubinafsishaji wa hoteli ya Golf, lengo kuu linasalia kuwa kuimarisha sekta ya utalii.

Waziri Mutua alizungumzia pia kuimarika kwa thamani ya sarafu ya Kenya ikilinganishwa na Dola ya Marekani akigusia umuhimu wake katika kuimarika kwa uchumi wa nchi hii.

Kuhusu elimu Mutua alidhihirisha matumaini yaliyo katika mtindo unaoibuka wa kutoa fursa sawa kwa mtoto wa kike na uzuri wake kwa jamii katika siku za usoni.

Waliohudhuria hafla hiyo ya tuzo katika shule ya Zayed ni seneta wa Mombasa Mohammed Faki na waziri wa elimu katika serikali ya kaunti ya Mombasa Daktari Mbwarali Kame kati ya wengine.

Share This Article