Serikali ya Ufaransa imepata pigo baada ya Waziri Mkuu Michel Barnier kuondolewa madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge waliunga mkono hoja hiyo kwa wingi miezi mitatu tu tangu Barnier kuteuliwa kuhudumu kwenye wadhifa huo na Rais Emmanuel Macron.
Vyama vya upinzani ndivyo viliwasilisha hoja ya kumbandua Barnier madarakani, kiongozi huyo ambaye awali alihusika kwenye mazungumzo ya kujiondoa kwa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.
Walimlaumu kwa kutumia nguvu zake spesheli kulazimisha kupitishwa kwa bajeti yake kwa njia ya utata bila kupigiwa kura.
Hii ndio mara ya kwanza serikali ya Ufaransa inaporomoka kupitia kura ya kukosa imani na kiongozi tangu mwaka 1962.
Hatua hii inazidisha ukosefu wa uthabiti wa kisiasa nchini humo, baada ya uchaguzi wa ghafla mwezi juni na Julai kuishia katika hali ya kila kundi kukosa wingi wa wabunge.
Katika kura hiyo ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, wabunge walihitajika kusema ndio au kususia kura. Kura 288 ndizo zilihitajika kupitisha hoja hiyo.
Jumla ya wabunge 331 walipiga kura ya ndio na sasa Barnier anafaa kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais Macron na bajeti iliyomsababishia madhila sasa imetupiliwa mbali.
Huenda akaendelea kukaa madarakani kwa muda, Macron anapotafuta mrithi wake.