Usalama wa chakula nchini umeimarika mno kwani idadi ya watu wanaokumbwa na ukame imepungua kutoka watu milioni 4.4 hadi milioni 2.8.
Hii ni kutokana na mvua za kutosha zilizonyesha kati ya mwezi Machi na Mei mwaka huu.
Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC Rebecca Miano alizindua ripoti ya mwaka 2023 kuhusu athari ya mvua za muda mrefu na usalama wa chakula nchini katika ofisi za Halmashauri ya Maendeleo ya Ewaso Ng’iro mjini Narok.
Katika utafiti uliofanywa kati ya Julai 10 na 21 mwaka huu, Miano amesema hali ya usalama wa chakula katika kaunti 23 zinazokumbwa na ukame iliimarika kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, ripoti hiyo iliashiria kuwa hali ya chakula katika kaunti za Turkana, Marsabit na Mandera inasalia kuwa “mbaya.”
Idadi ya kina mama wanaonyonyesha watoto wanaokabiliwa na utapiamlo pia ilipungua kutoka kina mama 144,914 mwezi Februari hadi 142,179.
Waziri alihusisha hatua hiyo na juhudi zilizoongezwa za kushughulikia suala la lishe na hali ya usalama wa chakula nchini.
Licha ya ufanisi huo, viwango vya utapiamlo bado vipo juu katika baadhi ya kaunti kame kama vile Turkana hasa maeneo ya Turkana Kusini na Horr Kaskazini, Marsabit, West Pokot, Mandera, Isiolo, Tana River na Baringo.
Ripoti hiyo pia iliashiria kuwa watu milioni 2.3 wanahitaji msaada wa chakula katika katika kaunti 23 zinazokumbwa na ukame.