Waziri Mbadi: Kenya ina akiba ya kutosha ya mafuta

Amedokeza kuwa serikali pia inafikiria kupitia upya VAT ili kuwakinga Wakenya dhidi ya kupanda kwa bei za mafuta ikiwa mgogoro wa Mashariki ya Kati utaendelea.

radiotaifa
2 Min Read

Taarifa ya Martin Mwanje na Abdiaziz Hashim

Waziri wa Fedha John Mbadi amewataka Wakenya kutoingiwa na hofu akisema nchi hii ina akiba ya kutosha ya mafuta. 

Akizungumza leo Alhamisi alipofika mbele ya Kamati ya Bunge juu ya Fedha na Mipango ya Kitaifa, Mbadi alisema serikali pia inafikiria kupitia upya Ushuru wa Thamani wa Ziada (VAT) ili kuwakinga Wakenya dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta ikiwa mgogoro wa Mashariki ya Kati utaendelea.

Kulingana na Waziri huyo, kufikia Machi 30, Kenya ilikuwa na tani metriki 138,623 za mafuta ya petoli yanayoweza kudumu siku 16,  tani metriki 207,841 za mafuta ya dizeli yanayoweza kudumu siku 19 na tani metriki 150,398 za mafuta ya ndege yanayoweza kudumu siku 49.

Aliongeza kuwa mafuta yanayotarajiwa kuwasili nchini kwa matumizi ya mwezi Machi hadi Aprili ni tani metriki 290,000 za mafuta ya petroli yatakayotumika kwa siku 47, tani metriki 182,900 za mafuta ya dizeli yatakayotumika kwa siku 20 na tani metriki 60,000 za mafuta ya ndege yatakayotumika kwa kipindi cha siku 25.

Serikali pia imeweka mipango ya kuagiza tani metriki 510,000 za mafuta ya petroli, 765,000 za mafuta ya dizeli na 200,000 za mafuta ya ndege yatakayotumika kati ya kipindi cha mwezi Mei hadi Julai.

Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umeathiri usafirishaji wa mafuta duniani kote na kusababisha kupanda kwa bidhaa hiyo katika mataifa mengi.

Katika nchi jirani ya Tanzania, bei ya mafuta imepanda kwa shilingi 50 za Kenya sawia na shilingi 1,000 za nchi hiyo kwa lita.

Shinikizo linazidi kutolewa kwa nchi za Marekani na Israel kusitisha mashambulizi nchini Iran ili kuleta uthabiti katika usambazaji wa mafuta duniani.

Share This Article