Waziri wa kilimo Mithika Linturi ameomba wakenya wawe na subira, wakati serikali ya Kenya Kwanza inatekeleza juhudi za kuhakikisha gharama ya maisha inapungua.
Akizungumza huko Igembe Kusini kaunti ya Meru kwenye hafla ya kutoa shukrani, Mithika aliwataka wakulima kutumia mvua inayoendelea kunyesha kupanda vyakula ili kuhakikisha uwepo wa chakula cha kutosha nchini.
Linturi alisihi watu pia waridhike na uongozi wa Rais Ruto unaolenga kuhakikisha kwamba mkenya wa kawaida anahisi kwamba serikali inamjali hawa wa mapato ya chini kama wakulima ambao mapato yao ni ya chini.
Alisema serikali imehakikisha gharama ya maisha inapungua kila siku kupitia uzalishaji wa chakula kwa wingi jambo ambalo lilisababisha upinzani usitishe maandamano ya kulalamikia gharama ya juu ya maisha.
Kulingana na waziri huyo, wakulima wa majani chai wamepata malipo ya kiwango cha juu chini ya serikali ya Kenya Kwanza.
Kuhusu madeni, Mithika alisema nchi hii haiwezi kuyategemea kukuza uchumi na ndio sababu serikali inatafuta namna ya kuyalipa.
Ombi lake kwa wakenya ni kwamba kila mmoja awajibike katika kuhakikisha nchi inasonga mbele.
Matamshi ya waziri Mithika yalikaririwa na viongozi kadhaa waliohudhuria hafla hiyo akiwemo mbunge wa Imento Kaskazini Rahim Dawood na wa Igembe ya kati Dan Kiiri.