Waziri wa Biashara Moses Kuria amesema hataridhia ombi la Waziri wa Kilimo Mithika Linturi la kuahirisha uzinduzi wa kituo cha viwanda katika kaunti ya Meru.
Kupitia mtandao wa X, Waziri Kuria alitetea uamuzi wake akisema tatizo la ukosefu wa ajira kati ya vijana haliruhusu subira ya aina yoyote hasa ya kutatua masuala ya kisiasa.
Alidokeza kuwa Waziri Linturi alimwomba aahirishe mpango huo kwa sababu ya matatizo ya kisiasa yanayokumba kaunti ya Meru.
Wawakilishi wadi wa kaunti hiyo wanapanga kuwasilisha bungeni hoja ya kumwondoa afisini Gavana Kawira Mwangaza.
Kuria anasema ameshazindua ujenzi wa vituo vya viwanda katika kaunti zingine kama vile Busia, Kakamega, Bungoma, Trans Nzoia, Migori, Siaya, Kisii, Nyamira, Mombasa, Kajiado, Narok na Laikipia, na sasa ni zamu ya kaunti ya Meru.
Joto la kisiasa limekuwa likiongezeka katika kaunti ya Meru katika siku za hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alilazimika kuingilia kati na kupiga marufuku mikutano yote ya Gavana Mwangaza chini ya mpango wake kwa jina “Okolea”.
Mkutano wake mmoja ulikumbwa na ghasia ambapo vijana waliokuwa na ghadhabu walichoma magodoro ambayo Mwangaza alikuwa amegawia wananchi na wakachinja ng’ombe wa maziwa ambaye alikusudiwa kufaidia familia moja na baadaye kugawana nyama.