Waziri Kindiki: Serikali kutumia elimu kumaliza vita, wizi wa mifugo Bonde la Ufa

Dismas Otuke
2 Min Read

Serikali imehiari kutumia elimu kama njia mwafaka ya kumaliza vita, wizi wa mifugo na utovu wa usalama katika eneo la kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Serikali inapania kuanzisha miradi kadhaa ya kutoa elimu katika eneo hilo, ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya ya shule na kutoa vifaa vya masomo kwa wanafunzi kwa shule zilizopo.

Kulingana na Waziri wa Usalama wa  Taifa Prof. Kithure Kindiki, mbinu hiyo itatoa fursa kwa watoto kutoka jamii zinazoathiriwa na wizi wa mifugo na vita vya mara kwa mara, kupata elimu na kutafuta mbinu mbadala za kujiimarisha kimaisha.

“Ili kuleta amani ya kudumu, tutajenga shule tano maalum ili
watoto kutoka jamii mbalimbali ikiwemo Pokot, Marakwet, Turkana waweze kusoma pamoja, kukaa pamoja na kushirikiana ili watusaidie kuwa na amani hata siku za usoni,” amesema Kindiki.

Wizara ya Usalama wa Taifa imeshirikisha serikali za kaunti za kaunti na wabunge  ili kufaniksiha mbinu hiyo ambayo inatarajiwa kurejesha amani na kufungua nafasi za ajira kwa wakazi.

Mpango huo pia utashirikisha mashirika ya serikali, sekta ya kibinafsi na wasomi  kutoka sekta mbalimbali watakaotoa hamasisho kwa jamii.

Kindiki amesema kuwa shule 15 zilizoharibiwa na wezi wa mifugo na majangili katika eneo bunge  la Tiaty zitajengwa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata masomo bila kutatizwa.

Serikali  pia imeongeza uwekezaji wake katika ujenzi wa vyuo vya kutoa mafunzo ya kiufundi  na vyuo vikuu vya kutoa mafunzo maarufu kama Satelite Campuses.

Waziri huyo ameelezea imani yake kuwa elimu ndio suluhu pekee kwa changamoto za usalama katika eneo la Bonde la Ufa.

 

Share This Article