Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, ametoa wito kwa wakazi wa kaunti ya Lamu kukumbatia amani na kukataa juhudi zozote za kukuza uhasama miongoni mwao.
Waziri huyo ambaye yuko kwa ziara ya kukadiria hali ya usalama katika kaunti ya Lamu, alisema uwepo wa tamaduni na dini tofauti ni nguzo muhimu katika ustawi wa taifa.
Aidha Kindiki aliwaonya baadhi ya viongozi waliochaguliwa ambao wanaangaziwa na serikali kwa kushukiwa kuwa wanachochea ghasia.
“Mkono wa sheria utamkamata yeyote atakayepatikana bila kujali vyeo vyao katika jamii au miegemeo yao ya kisasa,” alisema Kindiki.
Ziara ya Kindiki inajiri siku chache baada ya maafisa wa vikosi vya ulinzi hapa nchini KDF kujeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi waliokuwa wakipiga doria.
Maafisa wa usalama wametoa wito kwa wakazi kutoa habari kwa asasi za usalama kuhusu watu wanaowashuku kutekeleza uhalifu.