Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki anaongoza mkutano wa usalama katika eneo la Loruk, eneo bunge la Baringo kaskazini.
Mkutano huo na maafisa wakuu wa usalama wa eneo la Rift Valley na wale wa kaunti ya Baringo, pamoja na kamati za ujasusi, unalenga kubuni mipango ya kukabiliana na majangili wanaowahangaisha wananchi.
Ziara hiyo ya waziri Kindiki katika eneo hilo ambalo limeshuhudia mashambulizi ya magaidi, inajiri siku chache baada ya majangili kushambulia kambi ya maafisa wa polisi wa kikosi cha GSU, ambao walikuwa katika doria ya kawaida.
Majangili hao pia walishambulia shule moja karibu na kambi hiyo ya GSU, kabla ya kukabiliana na maafisa wa polisi.
Majangili hao waliokuwa wamejihami, walizingira kambi ya maafisa wa polisi wa GSU kuanzia saa nne asubuhi na kusababisha hofu kubwa katika kijiji cha Kapindasum.