Mbunge wa eneo bunge la Chesumei kaunti ya Nandi Paul Kibichiy, ametoa wito kwa waziri wa utumishi wa umma Justin Muturi, kujiuzulu na kukoma kutoa matamshi ya kuikashifu serikali ambayo anaitumikia.
Akizungumza alipokuwa akizindua miradi ya maendeleo katika eneo bunge la Chesumei, mbunge huyo alidokeza kuwa Muturi anapaswa kumheshimu Rais William Ruto na akome kukashifu juhudi za serikali ya Kenya Kwanza.
Waziri huyo alitakiwa kujiuzulu, kwa kuwa anapokea mshahara kutoka kwa serikali, lakini mchango wake katika utumishi wa umma ni duni.
Katika siku za hivi karibuni, Muturi amekuwa akielekezea kidole cha lawama serikali kutokana na visa vya utekaji nyara vijana, ambapo wengine wamepatikana wakiwa wameuawa.
Muturi alilaumu asasi za usalama hapa nchini kwa kumteka nyara mwanawe kwa madai ya kujihusisha na shughuli za ukosoaji serikali.