Waziri wa Afya Debora Barasa leo aliongoza shughuli ya kuhamasisha wakazi wa eneo la Moi’s Bridge katika kaunti ya Kakamega kuhusu usajili wao katika halmashauri inayosimamia bima ya afya ya jamii SHA.
Wakati wa shughuli hiyo, Barasa alihimiza wakazi hao kutumia fursa inayotolewa na usajili huo kupata huduma za afya.
Katika hotuba yake waziri Barasa alisisitiza jukumu muhimu linalotekelezwa na halmashauri ya SHA katika kulipia gharama ya matibabu na hivyo kupunguzia wagonjwa na familia zao mzigo wa kifedha.
Aliwataka wajisajili kwa wingi akisema bima ya afya ya jamii ina manufaa mengi kwa mtu binafsi na kwa jamii.
Mbunge wa eneo husika Innocent Mugabe, aliunga mkono matamshi ya waziri Barasa huku akiwataka wakazi kukumbatia halmashauri ya SHA na kujisajili huku wakijitenga na ukosoaji usiostahili.
Mugabe alimkosoa vikali aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, akimlaumu kwa kupinga mpango huo wa bima ya afya kwa manufaa ya kisiasa
Tony Nabwira, wa shirika la Posta naye pia aliunga mkono shughuli hiyo akisema SHA ni hatua muhimu katika kuafikia huduma zinazopatikana za afya na maslahi yaliyoimarishwa kwa jamii.
Aliwatia moyo waliohudhuria mkutano huo kujisajili bila kuchelewa na kuhamasisha wengine kuhusu umuhimu wa kujisajili.