Waziri Balaam Barugahara amtania Bajjo

Bajjo alichapisha picha za mwanamuziki aitwaye Laika kwenye mtandao wa X na kuziambatanisha na maneno yanayoashiria kwamba anammezea mate.

Marion Bosire
1 Min Read
Balaam Barugahara, Waziri, Uganda

Waziri wa masuala ya watoto na vijana nchini Uganda Balaam Barugahara, amemtania Bajjo ambaye ni mwandalizi wa matamasha ya muziki nchini humo kwenye mitandao ya kijamii.

Hii ni baada ya Bajjo kuchapisha picha za mwanamuziki Laika kwenye akaunti yake ya mtandao wa X huku akiziambatanisha na maneno yanayoashiria kwamba anammezea mate.

Bajjo ambaye jina lake halisi ni Alfonse Mukasa aliandika, “Ukweli ni kwamba mwanamke huyo ndiye mrembo zaidi nchini Uganda. Ni ndoto ya kila mwanaume. Ni ndoto yangu pia.”

Aliendelea kusema kwamba kwa umri alionao wa miaka 35, anastahili kuwa ameingia kwenye ndoa na kwamba akipatiwa fursa, Laika atakuwa mpenzi wake wa mwisho.

Alitania wanaume wakiwauliza iwapo kuna yeyote ambaye ana wivu kwake.

Waziri Barugahara, aliongeza maoni yake kwenye chapisho hilo ambapo aliandika, “Ninaogopa kwamba bosi wangu Madam Full Figure huenda akampiga jamani.”

Full Figure ambaye pia ni mwanamuziki wa kike aliwahi kufichua kwamba Bajjo ndiye baba ya mtoto wake lakini akafafanua tena kwamba alimwacha kwa sababu alikosa kuwajibikia mwanao.

Bajjo pia aliwahi kukiri kwenye mahojiano kwamba hana hisia tena kwa Full Figure ambaye jina lake halisi ni Jennifer Nakaggubi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *