Waziri wa Uchukuzi wa Afrika Kusini amesimulia jinsi alivyoibiwa kimabavu na majambazi waliokuwa wamejihami kwa bunduki baada ya kusimamisha gari lake barabarani ili kubadilisha gurudumi lililokuwa limeharibika.
Sindisiwe Chikunga aliambia kamati ya bunge kwamba mmoja wa majambazi hao aliyekuwa amefunika uso wake, alimshikia bunduki kichwani kwenye kisa hicho kilichotokea juzi Jumatatu.
Majambazi hao waliibia simu na silaha za walinzi wake.
Polisi walithibitisha kisa hicho wakisema msako mkali umezinduliwa dhidi ya majambazi hao kulingana na shirika la habari la AFP, lililomnukuu msemaji wa polisi Brigedia Athlenda Mathe.
Ikitaja njia moja ambayo hutumika na wahalifu, Wizara ya Uchukuzi nchini humo ilisema magurudumu ya gari la waziri huyo yalitobolewa na vyuma vilivyokuwa vimewekwa barabarani na majambazi hao ili kulazimisha gari hilo kusimama.
Afrika Kusini imekuwa na changamoto kubwa ya kukabili visa vya wizi wa magari, utekaji nyara wa watu pamoja na visa vingine ya ujambazi.