Wakati wakenya katika sehemu mbali mbali za nchi walikuwa wanajishughulisha na upanzi wa miche ya miti kulingana na pendekezo la serikali, waziri wa ardhi Alice Wahome aliongoza shughuli hiyo katika kaunti ya Laikipia.
Katika hotuba yake, waziri Wahome alisema kwamba shughuli hiyo itasababisha usawazishaji kimazingira na kustawisha uchumi kwani miti ina thamani kiuchumi.
Wahome aliwasihi wakazi wa kaunti ya Laikipia kujizoesha kupanda miti katika makazi na mashamba yao, shule na makanisa ili kuafikia lengo la serikali la miti milioni 250 katika muda wa miaka 10.
Matamshi sawia yalikaririwa na Gavana Joshua Irungu na mwakilishi wa kike wa kaunti hiyo Jane Kagiri ambao walisema kwamba Januari mwakani wataanzisha mipango ya upanzi wa miche ya miti katika shule zote za eneo hilo.
Waziri Wahome alitoa onyo kali dhidi ya watu ambao hukata miti kinyume cha sheria akisema kwamba serikali haitakubalia vitendo kama hivyo bila kufahamisha idara husika.