Wazee wa Njuri Ncheke wakataa kutatua mgogoro wa Gavana Mwangaza na wawakilishi wadi

Marion Bosire
1 Min Read

Baraza la wazee la jamii ya Ameru Njuri Ncheke limekataa kutatua mgogoro ulipo kati ya Gavana Kawira Mwangaza na wawakilishi wadi waliowasilisha hoja ya mjadala wa kumng’atua mamlakani kwa mara nyingine.

Mahakama kuu ya Meru katika uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na Mwangaza ya kukomesha mjadala huo, iliamua kwamba baraza la Njuri Ncheke lisuluhishe mgogoro uliopo.

Wazee hao wa jamii ya Ameru wamesema kwamba wao hushughulikia tu masuala ya kiraia na wala sio masuala sugu ya kikatiba kama mijadala ya kuondoa viongozi mamlakani.

Wamesema pia kwamba hawakutuma wakili mahakamani kuwawakilisha katika kesi hiyo ya Gavana Mwangaza.

Wametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakili aliyejisingizia kuwawakilisha mahakamani kwenye kesi hiyo kupitia kwa wakili wao halali.

Wakili huyo halali amejukumiwa pia kuwasiliana na mahakama huu ya Meru kuhusu uamuzi wao wa kutotatua mgogoro wa Gavana Mwangaza na wawakilishi wadi.

Kuhusu kazi waliyopatiwa na Rais Ruto ya kuhimiza umoja na utulivu kati ya viongozi wa kaunti ya Meru, baraza hilo linasema limetayarisha ripoti.

Kilichosalia kulingana nao ni kupatiwa tarehe ya kuwasilisha ripoti hiyo kwa kiongozi wa nchi kabla ya kupatikana kwa umma.

Share This Article