Wazee wa jamii ya Bukusu wahimiza umoja Trans Nzoia

Marion Bosire
2 Min Read
Mzee Peter Masinde

Wazee wa jamii ya Bukusu wanahimiza maelewano na umoja katika kaunti ya Trans Nzoia wakiwataka wakazi wa kaunti hiyo kujitenga na siasa za mgawaniko na waungane ili kuboresha jamii yao.

Wakizungumza na wanahabari mjini Kitale leo, wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti Peter Masinde, walisisitiza umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani kati ya watu wote wa kaunti.

Wamelalamikia jaribio la watu fulani la kupanda mbegu za mafarakano na kurudisha nyuma juhudi za kuhakikisha umoja.

“Kwa miezi kadhaa, viongozi fulani wenye nia mbaya, wamekuwa wakisabaisha ugomvi kati ya jamii zinazoishi katika kaunti hii.” alisema Masinde akiongeza kwamba wanalaani vitendo hivyo.

Aliwataka viongozi wote wa kaunti ya Trans Nzoia pasi na kuzingatia vyama vyao vya kisiasa watekeleza juhudi za kuleta amani na utangamano.

Wazee hao wanasisitiza umuhimu wa kutatua migogoro kupitia njia za kinyumbani na kuepuka utatuzi unaotoka nje ambao unaweza kusababisha mvutano.

Hawataki siasa pia ziingizwe katika utambulisho wa kikabila kwani njia kama hizo za kugawanya huathiri maendeleo.

Masinde alifafanua kwamba jamii ya Sabaot haijatengwa kwani viongozi kama mwakilishi wa kike na seneta wanatoka katika jamii hiyo na wengine wanashikilia nyadhifa mbali mbali katika serikali ya sasa.

Mzee Ferdinand Wanyisia alikuwa na maoni sawia huku akiambatanisha maendeleo yanayopatikana katika kaunti ya Trans Nzoia na bidii ya Gavana Natembeya.

Share This Article