Rais William Ruto ametoa wito kwa Wawakilishi Wadi wa muungano wa Kenya Kwanza kuelewa manifesto ya muungano huo ili wawaelezee Wakenya mashinani yaliyomo.
Amesema serikali inatekeleza mipango kadhaa inayolenga kubadilisha maisha ya Wakenya. Alitoa mfano wa mbolea ya bei nafuu, afya kwa wote, nyumba za gharama nafuu na vituo vya teknolojia ya habari na mawasiliano miongoni mwa mipango mingine.
Akielezea kuwa baadhi ya wakulima hawajapokea mbolea ya bei nafuu kwa sababu hawajajisajili, Rais Ruto aliwataka Wawakilishi Wadi hao kuongoza zoezi la usajili wa wakulima katika wadi zao.
“Tutahakikisha kila eneo linapata mbolea ya kutosha. Lengo letu ni kuongeza uzalishaji wa chakula na kuangamiza baa la njaa,” aliongeza Rais Ruto.
Aliyasema hayo leo Jumatatu alipofanya mkutano wa mashauriano na Wawakilishi Wadi wa muungano wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi.