Wawakilishi Wadi katika Bunge la kaunti ya Kiambu wamesitisha kwa kauli moja mjadala na upitishaji wa Mswada wa Fedha uliowasilishwa kwao na serikali ya kaunti hiyo.
Wametoa sababu mbalimbali za kuchukua hatua hiyo wanazotaka zinagaziwe kabla ya kuujadili na kuupitisha mswada huo.
Mswada huo uliwasilishwa na kiongozi wa wengi Gabriel Mucheke.
Hata hivyo, haukupokelewa vyema na wawakilishi wadi hao waliosema hawangeupitisha kwani kuna miswada ambayo ilipitishwa awali lakini serikali ya kaunti hiyo ilikataa kimakusudi kuichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali.
Walitoa mfano wa miswada ya vileo na ukadiriaji iliyopitishwa lakini Gavana Kimani Wamatangi amekataa kuichapisha kwa zaidi ya kipindi cha miezi sita iliyopita.
Akitoa uamuzi, Spika Charles Thiong’o aliahirisha vikao vya bunge hilo hadi mwezi Februari mwakani na kuzitaka kamati zilizo na masuala yanayopaswa kujibiwa kufanya mashauriano na kuyatatua.