Wavumbuzi wa Kenya kupokea ruzuku kutoka kwa ICANN

Marion Bosire
2 Min Read

Wavumbuzi nchini Kenya wana kila sababu ya kutabasamu kwani sasa wataweza kunufaika kutokana na hazina ya dola milioni 10 sawa na shilingi bilioni 1.6 za Kenya kutoka kwa shirika la ICANN.

Shirika hilo la kimtandao linalosimamia na kufanikisha ustawishaji wa tovuti na majukwaa mengine ya mtandao limetangaza ruzuku hiyo ya kimataifa leo.

Ruzuku hiyo inalenga miradi inayohimiza mbinu jumuishi na wazi katika kuendeleza mfumo wa mtandao wa utambuzi wa kipekee ulio imara, rahisi kutumia na salama.

Hii ni awamu ya kwanza ya ruzuku hiyo mpango ambao hatimaye utasambaza dola milioni 210
sawa na shilingi bilioni 33.6 za Kenya.

Upatikanaji wa mtandao unaimarika kila siku kote nchini hasa katika mataifa yanayostawi kama Kenya na kulingana na muungano wa kimataifa wa mawasiliano ya simu watu bilioni 5.3 kote ulimwenguni walikuwa wanatumia mtandao kufikia mwaka 2022, kiwango cha ukuaji cha asilimia 6.1 ikilinganishwa na mwaka 2021.

Rais wa muda wa ICANN ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji Sally Costerton anahisi kwamba jinsi teknolojia inazidi kuibukia, biashara na mifumo ya usalama ni muhimu njia za kipekee za utambuzi nazo zikue.

“Mpango wa ruzuku wa ICANN unatoa njia mpya ya kuendeleza juhudi hizo kwa kuwekeza katika miradi
ambayo imejitolea na inayounga mkono maono ya ICANN ya kuwa na mtandao mmoja ulio wazi na ambao unaweza kutumiwa na wote na unaoimarisha ujumuishaji kati ya jamii kubwa ya watumizi ulimwenguni.” alisema Sally.

Awamu ya kwanza ya ruzuku hiyo inaanza kutolewa Machi 2024 ambapo maombi yataanza kupokelewa tarehe 25 za mwezi huo wa tatu na kufungwa Mei 24, 2024 huku watakaonufaika wakitangazwa Januari 2025.

Masharti ya ustahiki wa ruzuku hiyo yanapatikana kwenye : https://icann.org/grant-program

Share This Article