Wavulana wawili wanauguza majeraha mabaya katika hospitali ya Thika level 5 baada ya kugongwa makusudi na gari la walinzi wa kampuni ya Del Monte Jumamosi asubuhi kwa kushukiwa kuiba mananasi.
Wawili hao wa umri wa miaka 17 kutoka Gatanga kaunti ya Kiambu Brian Ingusu na binamu yake David Lucheri, walikuwa kwenye pikipiki wakielekea nyumbani katika kijiji cha Kihiu Mwiri kutoka kutafuta chakula cha mifugo walipokimbizwa na gari hilo la walinzi.
Walinzi hao walisema vijana hao wamekuwa wakiiba mananasi kutoka kwa shamba la kampuni hiyo.
Ingusu ana majeraha mabaya kwenye uso na amevunjika ubavu na mguu wa kulia huku David akijeruhiwa uso mikono na miguu. Ingusu anasema gari hilo liliwagonga kutoka nyuma.
Wazazi wa vijana hao sasa wanaitaka kampuni ya Del Monte iwajibike igharimie matibabu ya wawili hao huku wakilalamikia uzembe wa wahudumu katika hospitali ya Thika Level 5 katika kushughulikia watoto wao.
Kulingana na jamaa za vijana hao, walinzi wa kampuni ya Del Monte kwa ushirikiano na maafisa wa polisi kutoka vituo vya polisi vilivyo karibu wamekuwa wakitekeleza visa kama hivyo kwa kushuku watu kuwa wezi.