Wauguzi katika Kaunti ya Isiolo wametia saini mkataba wa kurejea kazini na kukomesha mgomo wa miezi miwili uliosambaratisha huduma za afya katika hospitali zote za umma.
Hatua hiyo iliafikiwa baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya Chama cha Wauguzi nchini (KNUN), Bodi ya Huduma za Umma ya Kaunti na Serikali ya Kaunti, yaliyongozwa na Afisa wa Leba wa Kaunti hiyo Florence Karimi Mwenda.
Akihutubia wanahabari Jamatatu katika afisi za Bodi ya Huduma za Umma za Kaunti ya Isiolo, mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wauguzi Joseph Ngwasi na Katibu wa Tawi la Isiolo Martin Muse, walitangaza kuwa mgomo huo ulioanza Agosti 8,2025, sasa umesitishwa rasmi.
Walisema kuwa wauguzi wote katika vituo vya afya vya umma katika kaunti hiyo wanatakiwa kurejea kazini kufikia saa mbili asubuhi siku ya Alhamisi, Oktoba 16,2025.
Kwa wale waliokuwa wamesafiri mbali, walielezwa kuwa na muda wa saa 48 kufanya mipango ya kusafiri na kurejea kazini kufikia siku ya Alhamisi asubuhi.
Muse alibainisha kuwa malalamiko yote waliyoibua kwa mwajiri wao, ikiwa ni pamoja na kuajiri wauguzi zaidi ili kupunguza mzigo wa kazi na kuongeza ufanisi, kupandishwa vyeo kwa wauguzi waliokwama kwa miaka mingi katika makundi ya kazi yaleyale, na kutekelezwa kwa mkataba wa pamoja wa mwaka 2017, yote yameshughulikiwa kikamilifu na serikali ya kaunti, hivyo kupelekea chama hicho kukubali kusitisha mgomo huo.
Aidha, Muse alitoa pole kwa wakazi wa Isiolo kwa usumbufu walioupata wakati wa mgomo huo.
Katibu wa Kaunti ya Isiolo na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Dade Boru ambaye alimwakilisha Gavana Abdi Guyo pamoja na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Umma ya Kaunti, Joseph Mwangi Komu, walisema kuwa hakuna muuguzi atakayeadhibiwa kwa kutohudhuria kazi wakati wa mgomo.
Viongozi hao waliwahimiza wahudumu wa afya kuonyesha kujitolea na kujenga ari ya kutoa huduma bora za afya kwa wakazi wa Isiolo.
Pia waliwahimiza watumishi wa umma kupitia vyama vyao vya wafanyakazi kuzingatia mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro badala ya kuchukua hatua ya mgomo ambayo husababisha mateso kwa wananchi wasio na hatia.
Waliwataka wakazi wa Isiolo kuanza kutafuta huduma za afya katika vituo vya umma kuanzia Alhamisi asubuhi, wakisisitiza kuwa huduma zote zitarejea kama kawaida kufuatia kukamilika kwa mgomo huo wa miezi miwili.