Watunzaji misitu 118 wafuzu Kericho

Marion Bosire
1 Min Read

Wakenya 118 wamefuzu leo Jumatano kutoka taasisi ya kutoa mafunzo kuhusu misitu almaarufu Kenya Forestry College – KFC ambayo iko katika eneo la Londiani katika kaunti ya Kericho.

Akizungumza alipoongoza hafla hiyo ya 46 ya kufuzu, Waziri wa Mazingira na Misitu Soipan Tuya alisema kuwapa vijana ujuzi unaofaa pamoja na umilisi kutawasaidia kupata ajira katika sekta ya misitu sambamba na maono ya serikali ya Kenya Kwanza ya mpango wa kiuchumi wa Bottom Up na mkakati wa Wizara ya Misitu wa mwaka 2023 hadi 2027.

Waziri Tuya alisema vijana wenye ujuzi wanahitajika kuendeleza ajenda ya urejesho wa mazingira chini ya mpango wa upanzi wa miti bilioni 15 unaoongozwa na serikali wenye lengo la kuongeza eneo lenye misitu kufikia kiwango cha asilimia 30 kufikia mwaka 2032.

Waziri Tuya alikuwa ameandamana na Katibu wa Idara ya Misitu Gitonga Mugambi huku wenyeji wao wakiwa mtunzaji mkuu wa misitu Alex Lemarkoko, mwenyekiti wa bodi ya huduma ya misitu, KFS Titus Korir na mkuu wa taasisi ya KFC Dkt. Elizabeth Wambugu kati ya wengine.

Share This Article