Naibu Rais Rigathi Gachagua amewahimiza watumishi wa umma kuwaheshimu Wakenya huku wanapokabiliana na changamoto zinazokumba taifa hili.
Naibu Rais alisema Wakenya wanapaswa kuhudumiwa kwa heshima na kusikizwa kila wakati, hasa wakati huu mgumu wa kiuchumi.
“Sisi sote ambao tumepewa fursa ya kuwahudumia Wakenya, tunapaswa kufanya hivyo kwa unyenyekevu. Tunapaswa kuwaheshimu tunaowahudumia. Haikugharimu chochote,”alisema Naibu Rais.
Aliwataka wanaohudumu katika afisi za umma kuwa makini na jinsi wanavyowahutubia wananchi.
“Ikiwa unawahudumia Wakenya,bwao ndio waajiri wako. Unapaswa kuwaheshimu na jinsi unavyowahutubia.”
Wakati huo huo, Naibu wa Rais alisema serikali iko tayari kukabiliana na changamoto zinazohusiana na mvua ya El nino inayotarajiwa hapa nchini.
“Juma lijalo, nitaongoza mkutano wa kitaifa kuhusu maswala ya dharura pamoja na washirika wa kimaendeleo, serikali za kaunti, wizara husika na wadau wengine kutathmini jinsi tulivyo tayari,” alidokeza Gachagua.
Aliyasema hayo wakati wa kongamano la 36 la pamoja la baraza la kitaifa la kisayansi ya utafiti wa ugonjwa wa nagana mjini Mombasa.