Rais William Ruto leo Jumatano ameagiza Idara ya upelelezi wa maswala ya jinai (DCI) na tume ya Maadili na vita dhidi ya ufisadi EACC, kuwachukulia hatua maafisa wa umma waliotumia vyeti bandia vya masomo kuajiriwa.
“Wale ambao wamepata pesa kwa kutumia vyeti feki wanapaswa kujiuzulu na kurejesha pesa za umma,” alisema Rais Ruto.
Alisema serikali inajitahidi kujenga sekta ya umma ambayo ina sifa ya ufanisi wa hali ya juu, uadilifu, uwajibikaji na tija inayohitajika kwa Kenya kufikia matarajio yake ya maendeleo.
“Fadhila hizi pia ni muhimu ili kutimiza nia yetu ya kufanya Kenya kuwa bingwa wa uzalishaji barani Afrika na mwenyeji wa Kituo cha Tija cha Afrika,” aliongeza.
Akizungumza wakati wa Kongamano la tatu la mswada wa kitaifa wa ulipaji mishahara katika ukumbi wa bomas of Kenya Nairobi, Rais Ruto aliwataka viongozi wa taasisi za serikali kuunga mkono mageuzi ya SRC.
Hisia zake ziliungwa mkono na naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye alisema, katika nafasi yake kama mratibu wa tume za kikatiba na afisi huru, mageuzi yanayopendekezwa na SRC serikalini mara nyingi hukabiliwa na uhasama na kukataliwa.
“Napokea malalamiko na maombi mengi dhidi ya tume hii au ile; Asilimia 98 ya malalamiko na maombi yote ninayopokea ni dhidi ya mwenyekiti wa SRC,” akasema.
Wakati huo huo, Rais Ruto alipongeza taasisi zilizoshinda tuzo za uwajibikaji wa mswada wa mishahara kwa kutoa mfano mzuri kwa sekta nzima ya umma.
“Hii ndiyo njia ya kufuata, na mmedhihirisha kuwa inawezekana. Hongereni, na muendelee hivyo,” alisema.