Wafanyakazi wa serikali waonywa dhidi ya kuuza pombe Narok

Dismas Otuke
2 Min Read

Kamishna wa kaunti ya Narok Kipkech Lotiatia amewaonya watumishi wa umma dhidi ya kumiliki maduka ya kuuza pombe akitishia kuwatimua.

Akizungumza baada ya kuongoza msako mkali dhidi ya pombe haramu eneo la Majengo, Lotiatia alisema maafisa wa usalama wameimarisha vita dhidi ya pombe haramu hivyo basi maafisa wa serikali wanastahili kuwa mstari wa mbele kupambana na vileo haramu.

“Inakuwaje mtumishi wa umma anayepaswa kuwa mfano bora kwa wananchi anaendesha maeneo ya vileo? Wanachagua kubaki katika huduma au wafanye hiyo biashara,” alisisitiza.

Lotiatia alifichua kuwa magari yote yaliyokuwa yanasafiri kwenye barabara za kaunti hiyo yalikuwa yakikaguliwa ili kuthibitisha kuwa hayakuwa yakisafirisha pombe haramu.

Aliibua wasiwasi juu ya mtindo mpya ambapo wafanyabiashara katika sekta ya vileo wamehamishia biashara zao kwenye nyumba zao za kibinafsi na hivyo kuwa vigumu kwa vyombo vya usalama kutambua.

Hata hivyo, kamishna huyo alisema watatumia ujasusi zaidi ambao utasababisha kukamatwa kwa wale wanaoendesha shughuli zao katika nyumba zao za kibinafsi.

Wakati huo huo, aliwapongeza waendeshaji biashara ambao wamefunga biashara zao ambazo hazikuwa na leseni na kuchagua biashara mbadala.

“Tunafahamu kuwa baadhi ya watu wamehamia kwenye biashara nyingine ambazo zinaweza kuwapa faida nzuri na ni halali. Tunawahimiza wale wote wanaoendesha biashara za pombe haramu kuiga mfano huo na kufanya kazi halali zitakazowaingizia kipato.”

Watu watatu walikamatwa katika msako huo wa Majengo ambapo lita 10 za busaa na 10 za chang’aa ziliharibiwa.

Watatu hao walikuwa wakinywa pombe haramu na walipelekwa katika kituo cha polisi cha Narok huku wakisubiri kufikishwa kortini.

Msako huo unafuatia ziara ya Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kidiki, ambaye alitoa wito kwa maafisa wa usalama kuimarisha hatua za kuzuia unywaji wa pombe haramu.

Share This Article