Watu wengi wahama makazi yao kufuatia moto Los Angeles, Marekani

Moto huo mkubwa umeharibu nyumba kadhaa katika eneo la makazi ya kifahari na unasambaa haraka kutokana na upepo mkubwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Watu zaidi ya elfu 70 wamehamishwa kutoka eneo lililo na wakazi wengi la Los Angeles nchini Marekani kufuatia moto wa msitu ulioenea hadi kwenye eneo la makazi na kuteketeza nyumba nyingi.

Nyumba zipatazo elfu 1 zimeharibiwa na moto huo unaosambaa kwa kasi katika eneo la makazi ya kifahari la Pacific Palisades huko Los Angeles, kulingana na wahudumu wa zimamoto.

Rais wa Marekani Joe Biden amelazimika kutupilia mbali ziara yake nchini Italy ili aweze kushughulikia dharura hiyo ya moto, kulingana na taarifa kutoka ikulu ya White House.

Biden alikuwa amepangiwa kuondoka leo kuelekea Roma na Vatican, nchini Italia, safari zake za mwisho ughaibuni kabla ya kuachia madaraka baadaye mwezi huu.

Katibu wa ikulu Karine Jean-Pierre alisema katika taarifa kwamba Rais Biden ameidhinisha kutangazwa kwa hali hiyo ya moto kuwa dharura ya kitaifa.

Hasara iliyopatikana katika eneo hilo kufikia sasa kulingana na mtaalamu mmoja ni dola bilioni 50 huku wengi wa wakazi wakitibiwa kutokana na madhara ya kuvuta moshi kwenye hewa.

Daktari Puneet Gupta, mkurugenzi msaidizi wa huduma za matibabu katika kitengo cha zimamoto cha Los Angeles anasema kwamba hospitali za Los Angeles zina watu wengi wanaotaka huduma kutokana na kumeza moshi hali ambayo inaweza kusababisha mshtuko wa moyo na kuzidisha magonjwa ya pumu.

Haya yanajiri wakati ambapo vituo vya dharura vimelemewa na idadi kubwa ya watu na kuna uwezekano kwamba wagonjwa kwenye hospitali kadhaa watahitaji kuondolewa kwa sababu ziko katika hatari ya kukumbwa na moto huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *