Watu wawili wamekamatwa na maafisa wa polisi wakiwa na risasi 2,658 kinyume na sheria katika kaunti ya Laikipia.
Mwanamume na mkewe walikamatwa nyumbani kwao katika eneo la Minjore, kaunti ndogo ya Kirima kaunti ya Laikipia, baada ya maafisa wa usalama kupokea habari za kijasusi kutoka kwa wananchi.
“Polisi katika kaunti ya Laikipia jana tarehe 17 mwezi Aprili, walipata risasi 2, 658 katika nyumba ya Josphat Maina Karanja katika eneo la Minjore, kaunti ndogo ya Kirima,” ilisema taarifa ya polisi.
Kulingana na huduma ya taifa ya polisi kupitia mtandao wake wa X, washukiwa hao wawili wawili hao watafikishwa mahakamani leo Alhamisi.
Haya yanajiri huku serikali ikijizatiti kutwaa bunduki haramu zinazomilikiwa na majangili hasa katika maeneo ambako visa vya mashambulizi ya majangili vimekithiri.