Watu watatu wafariki baada ya ghasia kuzuka katika mpaka wa Kisumu-Kericho

Tom Mathinji
1 Min Read
Ghasia zazuka upya katika mpaka wa Kisumu na Kericho.

Watu watatu wameuawa baada ya kuzuka upya kwa mapigano kati ya jamii zinazoishi katika mpaka wa kaunti za Kisumu na Kericho.

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa baada ya wavamizi waliojihami kwa silaha hatari kushambulia kijiji cha Kadiang’a mashariki, kaunti ndogo ya Nyakach.

Kamishna wa kaunti ya Kisumu Hussein Alassow Hussein, alisema maafisa zaidi wa polisi wamepelekwa katika eneo hilo kurejesha hali ya utulivu.

Kulingana na kamishna huyo wa kaunti, maafisa hao wa polisi watashirikiana na wenzao kutoka kaunti ya Kericho kuhakikisha usalama unadumishwa katika eneo hilo.

Gavana wa kaunti ya Kisumu Prof. Anyang Nyong’o, amelaani shambulizi hilo, akisema inasikitisha sana kupoteza maisha kupitia kisa kama hicho.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba kisa hiki kinajiri wakati ambapo Rais anatarajiwa kuzuru eneo hilo,”alisema Nyongó.

Gavana huyo aliwaagiza maafisa wa usalama kuwakamata waliotekeleza uovu huo, na kuhakikisha haki inapatikana kwa familia zilizoathiriwa.

Biashara katika mji wa Sondu zilitatizwa huku vijana waliokuwa na hamaki wakifunga barabara kulalamikia mauaji hayo.

TAGGED:
Share This Article