Watu wanne walifariki katika maandamano nchini Cameroon hususan mjini Douala, huku upinzani ukimtuhumu Rais Paul Biya kwa jaribio la kuiba kura.
Polisi na waandamanaji wa upinzani walikabiliana kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais, kwa mujibu wa gavana wa eneo hilo.
Makabiliano hayo ya Jumapili yalitokea baada ya mamia ya wafuasi wa mgombea urais wa upinzani, Issa Tchiroma kupuuza marufuku ya maandamano na kujitokeza barabarani mjini Douala.
Tchiroma anashikilia kwamba alipata kura nyingi zaidi ya Rais Paul Biya.
Waandamanaji walifunga barabara, wakachoma matairi na kurusha mawe na vitu vingine kwa polisi, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Polisi walijibu kwa kutumia vitoza machozi na magari ya maji ya kuwatawanya.
Samuel Dieudonne Ivaha Diboua, gavana wa eneo linalojumuisha Douala, aliambia shirika la habari la AFP kuwa waandamanaji hao walivamia vituo vya polisi katika wilaya ya pili na ya sita ya jiji hilo.
Aliongeza kusema kwamba baadhi ya askari walijeruhiwa, na watu wanne kwa bahati mbaya wakapoteza maisha.
Usimamizi wa kampeni ya Tchiroma pia umethibitisha vifo hivyo.
Maandamano hayo yalifuatia matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa Oktoba 12, yaliyoripotiwa na vyombo vya habari na kuonyesha kuwa Biya, wa umri wa miaka 92, alikuwa anakaribia kushinda muhula wa nane madarakani.
Lakini Tchiroma alidai kwamba alipata asilimia 54.8 ya kura dhidi ya 31.3 za Biya, na akatoa wito kwa watu wa Cameroon siku ya Jumatano kuandamana endapo Baraza la Katiba litatangaza matokeo yaliyopotoshwa na kughushiwa.
Serikali ya Cameroon imekanusha tuhuma za upinzani kuhusu dosari katika uchaguzi huo na kuwataka wananchi wasubiri matokeo rasmi yanayotarajiwa kutangazwa na Baraza la Katiba leo Jumatatu.

