Watu 4 wakamatwa Juja, Kiambu baada ya kuua mlinzi na kuiba pombe

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa polisi huko Juja kaunti ya Kiambu wamekamata washukiwa wanne wa wizi baada yao kuua mlinzi na kuiba pombe kutoka eneo moja la burudani lililofunguliwa hivi maajuzi.

Eneo hilo linafahamika kama “Midnight Gardens” na liko katika eneo la Kimbo.

Washukiwa hao walikuwa wamejihami kwa silaha mbali mbali walipovamia klabu hicho cha usiku leo alfajiri.

Walizima stima na mtambo wa jenereta, wakamfunga mlinzi huyo kwa kamba kabla ya kumuua kwa kutumia chuma.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Kiambu Michael Muchiri, anasema polisi walipata silaha walizotumia washukiwa hao ikiwemo bunduki bandia waliyotumia kutishia wahudumu wa eneo hilo la burudani katika kisa hicho cha saa 10 alfajiri.

Walikuwa tayari wameiba pombe ya thamani ya pesa nyingi ambayo wanaaminika kwenda kuuza katika maeneo mengine.

Mshukiwa mkuu John Maina anayemiliki maduka ya kuuza nyama huko Ruiru na Utawala na wenzake walikuwa wamepakia pombe hiyo kwenye gari aina ya Toyota Noah iliyokuwa na nambari bandia za usajili walipokamatwa.

Kulingana na Muchiri polisi wamekuwa wakifuatilia shughuli za genge hilo baada ya kupashwa habari na wakawawekea mtego.

Mshukiwa mmoja wa genge hilo anasakwa na polisi.

Meneja wa kituo hicho cha burudani kwa jina Jeff Wachira, alisema kwamba walipata hasara kubwa kwani walikuwa wamenunua pombe kwa wingi wezi hao walipowavamia.

Mwakilishi wa wadi katika eneo hilo Ngatha Wambiri anaomba serikali kuimarisha ulinzi katika eneo hilo kwa kuwapa polisi gari la kutumia wanaposhika doria.

Wambiri hata hivyo alipongeza polisi kwa kufika haraka katika eneo la tukio.

Share This Article