Watu wanne wamefariki baada ya shambulizi la bomu kutekelezwa katika kituo cha mazoezi cha Chuo Kikuu cha Mindanao mjini Marawi nchini ufilipino.
Kituo hicho cha mazoezi kilikuwa kinatumiwa kama kanisa ambapo misa ya Jumapili asubuhi ilikuwa ikiendelea.
Rais wa nchi hiyo Ferdinand Marcos Jr amelaani shambulizi hilo akisema ameagiza maafisa wa polisi na wale wa jeshi kuhakikisha usalama wa wananchi.
Rais Marcos alisema washambuliaji ambao wanatekeleza mashambulizi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, siku zote, watachukuliwa kuwa adui kwa jamii.
Gavana wa mkoa wa Lanao del Sur ambapo shambulizi hilo lilitokea Mamintal Alonto Adiong Jr, naye amelaani shambulizi hilo, akisema haki za kimsingi za watu huheshimiwa katika mkoa huo zikiwemo zile za kuabudu.
Alisema mashambulizi dhidi ya taasisi za masomo ni lazima yalaaniwe kwa sababu maeneo hayo huimarisha utamaduni wa amani na kukuza vijana kuwa viongozi wa baadaye wa nchi.
Chuo Kikuu cha Mindanao kimetoa taarifa pia kikisema kimetikiswa na shambulizi hilo na kwamba kimesimamisha masomo hadi itakapotangazwa tena.
Taarifa ya usimamizi wa chuo hicho ililaani kitendo hicho huku ikifariji jamii za waathiriwa wa shambulizi hilo.
Shahidi mmoja aliambia wanahabari kwamba alisikia mlipuko mkubwa kama ule wa mtambo wa stima almaarufu “transformer”.
Baadaye, aliona magari ya ambulensi na ya maafisa wa polisi ndani ya chuo hicho kikuu.
Polisi wanachunguza chanzo cha shambulizi hilo ukiwemo uwezekano kwamba lilitekelezwa na wanamgambo wanaoshirikiana na wale wa ISIL.