Watu wanne waliuawa, huku wengine 11 wakipata majeraha katika shambulizi linaloshukiwa kuwa la kigaidi kaunti ya Mandera.
Miongoni mwa walioaga dunia ni pamoja na maafisa watatu wa polisi na mwanamke mmoja baada ya kilipuzi kutokea katika hoteli moja, mjini Mandera.
Akithibitisha shambulizi hilo, Kamanda wa polisi kaunti ya Mandera Samuel Mutunga, alisema washukiwa wa shambulizi hilo, walitega kilipuzi hicho wakati wa usiku.
“Tunaamini kuwa washambuliaji hao walitega kilipuzi hicho wakati wa usiku,” alisema afisa huyo mkuu wa polisi.
Kulingana na Mutunga, watu wawili kati ya waliojeruhiwa walipata majeraha mabaya na wanapokea matibabu katika hospitali ya matibabu maalum ya Mandera, huku wakisubiri kusafirishwa hadi Jijini Nairobi kwa matibabu maalum.
Akilaani kisa hicho, kamanda huyo wa polisi aliwataka wakazi wa eneo hilo kutahadhari na kujiuepusha na mikusanyiko, huku akiwataka kuwaripoti wao ambao wana mienendo yakutiliwa shaka.
Alisema maafisa wa upelelezi wanachunguza swala hilo.