Watu wanne wameandikisha taarifa na maafisa wa upelelezi wanaochunguza mauaji ya wanawake wawili na msichana mmoja katika mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi.
Waris Daud, Amina Abdirashid na binamu yao aitwaye Nusuiba Dahir waliuawa kinyama, mauaji ambayo yameibua ghadhabu kati ya wakazi wa mtaa huo.
Walioandikisha taarifa wanajumuisha jamaa aliyekamatwa na kuzuiliwa na polisi ambaye ni mshirika wa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo.
Miili ya waathiriwa ilizikwa katika makaburi ya Lang’ata huku maafisa wa polisi wakizuru maeneo kadhaa yanayohusishwa na mauaji hayo.
Walifanikiwa kupata video ya CCTV ya kituo cha mafuta kwenye barabara ya Mombasa ambapo gari linaloaminiwa kutumika kusafirisha miili ya waathiriwa lilionekana likijazwa mafuta.
Uchunguzi unaonyesha kwamba mshukiwa aliweka gari hilo mafuta kwenye kituo hicho baada ya kutupa mwili katika eneo moja la kaunti ya Machakos.
Jamaa ambaye alikuwa akiwasiliana na mshukiwa mkuu wa mauaji usiku ambao yalitekelezwa na ambaye anaishi naye kwenye nyumba moja mtaani Eastleigh naye alihojiwa na polisi.
Mwingine aliyehojiwa ni mmiliki wa nyumba ambayo wawili hao wanaishi ambaye aliwakodisha bila hata ya kuitisha stakabadhi za utambuzi na nyingine.
Watu wawili zaidi waliouzia mshukiwa simu ya thamani ya shilingi elfu 23 katikati mwa jiji la Nairobi nao wamehojiwa na polisi.
Video ya CCTV katika jengo moja mtaani Eastleigh inayoonyesha mwathiriwa wa mauaji kwa jina Warris Said Daud akiwa na mshukiwa mkuu usiku ambao mauaji yalitekelezwa pia imeangaliwa na polisi.
Uchunguzi ulipanuliwa hadi eneo la Bahati huko Buruburu, ambapo ushahidi zaidi ulikusanywa.
Jamaa anayemfanana mshukiwa wa mauaji alikamatwa katika eneo la Dhobley nchini Somalia, na kuachiliwa baada ya mahojiano makali na polisi.
Waathiriwa waliombewa kwenye msikiti wa Al Noor mtaani South C kabla ya miili yao kuzikwa Lang’ata.