Watu saba wafariki baada ya mgodi kuporomoka Siaya

Tom Mathinji
1 Min Read
Kaka wawili wauawa Kakamega.

Watu saba wamethibitishwa kufariki huku wengine wanne wakipokea matibabu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Bondo baada ya mgodi kuporomoka na kuwazika wakiwa hai katika kijiji cha Lumba, kaunti ndogo ya Rarieda jana Jumanne asubuhi.

Kisa hicho kilitokea saa tano asubuhi katika migodi ya dhahabu ya Kasweto katika kata ya Ramba Kaskazini.

Kamanda wa polisi kaunti ya Siaya Cleti Kimaiyo alithibitisha kisa hicho, akisema manusura wanne walikimbizwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi.

Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Rarieda Kennedy Lunalo alisema wachimbaji hao wa migodi walienda kinyume cha maagizo yaliyositisha uchimbaji madini katika eneo hilo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Lunalo alisema imekuwa ni changamoto kwa uongozi kuhakikisha kuwa agizo la kusitisha uchimbaji linazingatiwa kwa vile nyumba nyingi za eneo hilo zina nyufa.

Hata hivyo, alisema wataendelea kuwaonya wachimbaji katika eneo hilo kujiepusha na migodi hiyo hatari ili kuepusha majanga kama hayo siku zijazo.

Miili ya waathiriwa imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ndogo ya kaunti ya Bondo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *