Watu kadhaa walazwa hospitalini baada ya kula nyama ya ng’ombe aliyeugua kimeta

Marion Bosire
2 Min Read

Watu kadhaa wamelazwa kwenye hospitali mbalimbali huku wengine wakitibiwa na kuruhusiwa kuondoka baada ya kula nyama ya ng’ombe ambaye anaaminika kuugua kimeta huko Kigumo, kaunti ya Murang’a.

Mmiliki wa mnyama huyo Christopher Ngugi, alielezea alivyogundua ng’ombe wake mmoja alikuwa akiugua na kumfahamisha afisa wa afya ya wanyama katika eneo hilo.

Afisa huyo anasemekana kupasua mzoga wa ng’ombe huyo na kubaini kwamba alikuwa amemeza karatasi za plastiki na ndizo zilisababisha kifo chake.

Kutokana na hakikisho hilo, majirani wa Ngugi walifika nyumbani kwake kununua nyama ya ng’ombe huyo ambayo aliwauzia kwa shilingi 400 kwa kilo ilhali bei katika maduka ya nyama ni shilingi 600.

Muda mfupi baadaye waliosaidia katika kuchinja nyama hiyo walianza kuonyesha dalili za malengelenge na vidonda kwenye miguu na mikono.

Dalili sawia zilishuhudiwa kwenye miili ya waliokula nyama hiyo manyumbani na katika mahoteli ya eneo hilo.

Idadi ya walionunua nyama hiyo inakisiwa kuwa watu 150 na kushiriki mlo wake na wanafamilia wao na idadi jumla ya waathiriwa inakisiwa kuwa watu 600.

Serikali ya kaunti ya Murang’a sasa inaombwa kupeleka maafisa wa matibabu katika eneo la Kigumo kutoa huduma kwa waathiriwa kwani wengi wao hawawezi kumudu usafiri hadi hospitalini.

Maafisa wa afya ya wanyama pia wanaombwa kutoa dawa kwa wanyama wote wa eneo hilo ili kunusuru wakazi.

Website |  + posts
Share This Article