Watu 9 wafariki baada ya basi kutumbukia katika mto Mbagathi

Tom Mathinji
1 Min Read

Watu tisa wameripotiwa kufariki, huku wengine wakijeruhiwa,  baada ya basi lililokuwa likielekea Jijini Nairobi kutoka mtaa wa Karen kutumbukia katika mto Mbagathi.

Dereva wa basi hilo la abiria 33, linalomilikiwa na kampuni Naboka Sacco, anasemekana kupoteza mwelekeo, na kusababisha basi hilo kutumbukia mtoni.

Waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea leo Jumamosi saa nne asubuhi, walipelekwa katika vituo vya afya vilivyo karibu kwa matibabu.

Maafisa wa polisi na waokoaji, walifika katika eneo la mkasa, wote pamoja wakishirikiana kuwaokoa manusura.

Aidha maafisa wa polisi wameonya kuwa kuna msongamano mkubwa wa magari katika eneo hilo kufuatia ajali hiyo, huku wakiwataka madereva kutumia njia mbadala.

Kulingana na takwimu za NTSA, watu 1,553 wamefariki kati ya mwezi Januari na mwezi Aprili mwaka 2024, kupitia ajali za barabarani.

TAGGED:
Share This Article