Watu 5 wafariki katika ajali ya barabarani Gilgil

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu 5 wafariki katika ajali ya barabarani Gilgil.

Watu watano wamefariki baada ya kuhusika katika ajali kwenye barabara ya Gilgil kuelekea Naivasha.

Kulingana na maafisa wa polisi, watu wengine 19 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea wa saa moja unusu Alhamisi jioni.

Shirika la msalaba mwekundu lilisema maafisa wake walifika katika eneo la mkasa na kusaidia katika shughuli za uokoaji.

“Ajali ya barabarani imeripotiwa katika sehemu ya kupima uzani wa magari ya Gilgil, iliyohusisha matatu tatu,” ilisema taarifa ya shirika hilo.

Waliofariki walijumuisha wanaume wawili, mwanamke, mvulana na msichana. Kulingana na polisi, ajali hiyo ilihusisha gari aina ya matatu inayomilikiwa na kampuni ya Narok Line Services, matatu ya kampuni ya Mau Narok na nyingine ya kampuni ya Ennus.

Aidha polisi waliongeza kuwa gari moja lilikuwa likikokotwa na jingine kutoka Naivasha kuelekea Gilgil kabla ya ajali hiyo kutokea.

Gari hilo lilipoteza mwelekeo na kisha kubingiria mara kadhaa. Waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha.

Wakati uo huo, miili ya waliofariki ilipelekwa katika chumba cha wafu cha hospitali ya kaunti ndogo ya Gilgil.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article