Watu 33 wameuawa baada ya vijiji kadhaa kushambuliwa na watu waliokuwa na silaha, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Mamlaka na Makundi ya Kijamii yamesema kuwa wavamizi hao wanaodaiwa kuwa washirika wa kundi la ISIS, waliteketeza nyumba kadhaa na hospitali, huku wakiwaua raia.
Kulingana na msimamizi wa eneo la Beni Kanali Charles Omeonga, wavamihi hao waliteketeza hospitali iliyokuwa ikiwahudumia wagonjwa wa Ebola, na kusababisha wagonjwa hao kutoroka.
Miongoni mwa wale waliotoroka ni wagonjwa 180, miongoni wao waathiriwa wa Ebola, alisema Christian Kakule, mkurugenzi wa matibabu katika kituo cha afya cha Kelekele, eneo la Cantine.
Kiongozi wa kundi la kijamii Tchetche Aliamini, alithibitisha kuwa wengi wa waliouawa walipigwa risasi, wengine wakachomwa moto huku baadhi ya wengine wakikatwa kwa panga.