Takriban watu 30 wamefariki nchini Sudan na vijiji 20 kuharibiwa zaidi, baada ya bwawa Arbaat kuvunja kingo zake kutokana na mvua kubwa inayonyesha.
Mvua kubwa inayoshuhudiwa mashariki mwa Sudan, imesababisha mafuriko yaliyojaza maji hadi pomoni katika bwawa la Arbaat siku ya Jumapili, kilomita 40 kaskazini mwa Port Sudan.
Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, watu 50,000 wameathiriwa na mafuriko hayo, idadi hiyo ikijumuisha watu waliokuwa wanaishi magharibi mwa bwawa hilo na kwamba si rahisi kuwafikia watu walio mashariki mwa bwawa.
Bwawa hilo lilikuwa chanzo kikuu cha maji kwa ajili ya mji wa Port Sudan, unaokaliwa na watu wanaofanya shughuli zao kwenye bandari ya Bahari ya Shamu, na uwanja wa ndege, na kupokea misaada inayohitajika sana kwa ajili ya watu wa Sudan.