Maafisa wa utawala nchini Pakistan wamesema kuwa takriban watu 25 wameuawa baada ya bomu kulipuka katika kituo cha reli kwenye jimbo la Balochistan.
Wengine wengi walijeruhiwa katika mlipuko huo, ambao ulitokea wakati treni maarufu ya asubuhi ilikuwa inataka kuondoka kituo cha Quetta kusini magharibi ya Pakistan kuelekea Peshawar.
Afisa mkuu wa polisi Muhammad Baloch alisema mlipuko huo unakisiwa kusababishwa na mlipuaji wa kujitoa mhanga kufa aliyekuwa amebeba kati ya kilo 6 na 8 za vilipuzi. Miongoni mwa waliofariki na kujeruhiwa ni pamoja na raia na wanajeshi.
Kundi la wanamgambo kwa jina Balochistan Liberation Army, lilikiri kutekeleza shambulizi hilo ambalo polisi wamelichukulia kuwa shambulizi la kujitoa mhanga kufa.